KB
Kristo Bwana
OFFICIAL WEBSITE
← Latest Posts
Latest Post

MUNGU HATAZAMI HISTORIA YAKO, ANAANGALIA IMANI YAKO.

MUNGU HATAZAMI HISTORIA YAKO, ANAANGALIA IMANI YAKO.

UTANGULIZI.

Tutarejea kwa mwanamke mmoja katika biblia ambaye biblia inamtaja kuwa alikuwa kahaba.
Katika Biblia tunasoma habari za Rahabu, mwanamke aliyekuwa akiishi katika mji wa Yeriko na Biblia inamtaja kuwa kahaba.
Kwa mtazamo wa mwanadamu, Rahabu alikuwa na historia ambayo ingeweza kumfanya adharauliwe na kukataliwa. Lakini Mungu aliona kitu kingine ndani yake imani.
Rahabu aliposikia habari za Mungu wa Israeli, hakuishia kusikia tu; aliamini, akachukua hatua, akawapokea watumishi wa Mungu na akasimama upande wa Mungu.
Matokeo yake yalikuwa makubwa: Mungu alimwokoa yeye pamoja na nyumba yake, akamwingiza katika jamii ya watu wake, na hata akamfanya kuwa sehemu ya ukoo wa Yesu Kristo.
Hili ni fundisho kubwa kwetu: Historia yako inaweza kuwa mbaya, lakini Mungu anaweza kuandika ukurasa mpya wa maisha yako.

Yoshua 2:1 “...wakaingia nyumbani mwa mwanamke kahaba, jina lake Rahabu...”

MAMBO MAKUU MATATU(3) AMBAYO RAHABU ALIFANYA MUNGU AKAMHESABIA HAKI;

I. RAHABU ALIKUWA KAHABA, LAKINI ALISIKIA HABARI ZA MUNGU.
Biblia haifichi historia ya Rahabu. Inamtaja waziwazi kuwa alikuwa kahaba.
Lakini Mungu hakuruhusu historia yake iwe mwisho wa maisha yake.
Rahabu alisikia habari za mambo ambayo Mungu alikuwa amewatendea watu wake. Alisikia jinsi Mungu alivyowatoa katika utumwa na kuwashindia maadui zao.
Habari hizo zikazaa imani ndani yake.
Fundisho: Usidharau mtu anayesikia Neno la Mungu.
Mtu anaweza kuwa mbali na Mungu leo, lakini akasikia Neno na kesho maisha yake yakabadilika kabisa.
Usimhukumu mtu kwa hali yake ya sasa; Mungu anaweza kuwa anaanza kazi ndani yake.

Yoshua 2:10-11 “Kwa maana tumesikia jinsi BWANA alivyoyakausha maji ya Bahari ya Shamu... Kwa maana BWANA, Mungu wenu, ndiye Mungu juu mbinguni na chini duniani.”

II. RAHABU HAKUISHIA KUSIKIA-ALIAMUA KUAMINI.
Rahabu aliposikia habari za Mungu, alifanya uamuzi.
Aliamini kwamba Mungu wa Israeli ndiye Mungu wa kweli.
Imani yake haikuwa maneno tu. Aliamua kuchukua hatua.
Hii inatufundisha kwamba imani ya kweli humfanya mtu achukue hatua.

Waebrania 11:31 “Kwa imani Rahabu, yule kahaba, hakuangamia pamoja na wale walioasi, kwa kuwa aliwakaribisha wale wapelelezi kwa amani.”

III. RAHABU ALITAFUTA WOKOVU WAKE NA WA NYUMBA YAKE.
Rahabu hakutaka kuokoka yeye pekee.
Aliomba kwamba yeye na familia yake wahifadhiwe.
Aliwaomba wale wapelelezi wahakikishe kwamba baba yake, mama yake, ndugu zake na wote waliokuwa katika nyumba yake wanaokolewa. (Yoshua 2:12-13)
Hapa tunajifunza jambo muhimu:
Mtu anayekutana na Mungu kwa kweli hutamani wengine pia wamjue Mungu.

NEEMA ZA PEKEE AMBAZO RAHABU ALIPEWA NA MUNGU;
I. MUNGU ALIMWOKOA RAHABU PAMOJA NA FAMILIA YAKE.
Yeriko ilipoharibiwa, Rahabu hakuharibiwa pamoja na watu wa Yeriko.

Yoshua 6:25 “Lakini Yoshua akamhifadhi Rahabu, yule kahaba, na nyumba ya baba yake, na wote waliokuwa pamoja naye..

II. MUNGU HAKUMWOKOA TU BALI ALIMPA NAFASI MPYA.

Rahabu hakumalizia maisha yake katika historia ya Yeriko.
Aliingia katika maisha mapya pamoja na watu wa Mungu.
Jambo la kushangaza zaidi ni kwamba Mungu alimjumuisha katika ukoo wa Yesu Kristo.

Mathayo 1:5 “Salmoni akamzaa Boazi kwa Rahabu; Boazi akamzaa Obedi kwa Ruthu; Obedi akamzaa Yese.”

Hii ni neema kubwa sana.
Rahabu alikuwa kahaba, lakini Mungu alimfanya kuwa sehemu ya historia ya wokovu ambayo ilifikia kilele katika kuja kwa Yesu Kristo.
Hii inatufundisha nini?
Usimruhusu mtu akufafanue kwa historia yako wakati Mungu anaweza kukupa utambulisho mpya.

Mwanadamu anaweza kusema:
“Huyu ni yule kahaba.”
Lakini Mungu anaweza kusema:
“Huyu ni mwanamke mwenye imani".