UTANGULIZI.
Tunaposoma Sura ya 13 ya kitabu cha 1 Wakorintho inazungumzia sifa za upendo wa kweli. Paulo anaonyesha kwamba karama, elimu, unabii, na hata imani vina thamani ndogo ikiwa havina upendo. Moja ya sifa kubwa za upendo ni kwamba "huvumilia yote."
Neno "yote" lina maana ya kila jambo bila ubaguzi. Halimaanishi baadhi ya mambo au yale yanayotupendeza, bali linaonyesha kwamba upendo wa Mungu humwezesha mtu kuvumilia katika kila hali inayompata, akiwa na tumaini na imani kwa Mungu.
UPENDO HAUJICHAGULII MAMBO YA KUVUMILIA.
Upendo Haujichagulii Mambo ya Kuvumilia. Watu wengi huvumilia mambo yanayowanufaisha, lakini hukata tamaa yanapokuwa magumu. Biblia haifundishi hivyo.
Paulo hakusema: Upendo,
Huvumilia mambo mepesi.
Huvumilia yanayomletea faida.
Huvumilia yale anayoyapenda.
Alisema: Upendo,
"Huvumilia yote."
Hii inamaanisha:
Huvumilia majaribu.
Huvumilia mateso.
Huvumilia kukataliwa.
Huvumilia kukosolewa.
Huvumilia dhiki.
Huvumilia hata kuchelewa kwa majibu ya Mungu.
Mtu mwenye upendo wa Kristo habadiliki kwa sababu mazingira yamebadilika.
MKRISTO ANAPASWA KUWA MVUMILIVU KWA MAMBO YOTE.
Yesu Alifundisha Uvumilivu wa Mpaka Mwisho.
Yesu hakusema:
"Mwenye kuanza vizuri ataokolewa."
Hakusema:
"Mwenye kuvumilia kwa muda mfupi ataokolewa."
Alisema:
"Mwenye kuvumilia HATA MWISHO."
Safari ya wokovu si mbio za kasi bali ni mwendo wa kudumu katika Uvumilivu na uaminifu kwa Mungu hadi mwisho wa maisha.
UVUMILIVU NI ISHARA YA IMANI IMARA.
Uvumilivu ni Ishara ya Imani Imara. Mungu haruhusu majaribu ili kutuangamiza, bali kutukomaza.
Dhahabu hujaribiwa kwa moto ili iondoke na uchafu wake. Vivyo hivyo, Mkristo hupitia majaribu ili imani yake itakaswe.
Ayubu alipoteza:
Mali zake.
Watoto wake.
Afya yake.
Marafiki walimhukumu.
Mke wake alimkata tamaa.
Lakini hakumwacha Mungu. Ndiyo maana mwisho wake Mungu alimbariki kuliko mwanzo.
UPENDO WA MUNGU HUVUMILIA YOTE.
Upendo wa Mungu hauchagui mambo ya kuvumilia. Unavumilia yote kwa sababu unategemea nguvu za Mungu, si hisia za mwanadamu.